I made this widget at MyFlashFetish.com.

Wednesday, June 23, 2010

WAGOMBEA URAIS CCM WACHUKUA FOMU LEO

anachama Saba wa chama cha Mapinduzi CCM, tayari wamejitokeza kuchukua fomu za kuwania urais wa Zanzibar kwa tiketi ya chama hicho katika afisi kuu ya CCM Kisiwandui.

Wanachama hao ni waziri kiongozi Shamsi Vuai Nahodha, makamo wa rais Dr. Ali Mohammed Shein, waziri kiongozi wa zamani Dr. Mohammed Gharib Bilal na naibu waziri kiongozi Ali Juma Shamhuna.

Wengine ni naibu waziri wa Afrika mashariki Mohammed Aboud, balozi Ali Abeid Karume na kamishna mstaafu wa utamaduni Hamad Bakar Mshindo.

Wakizungumza na waandishi wa habari kwa nyakati tofauti wagombea hao wametaja kuimarisha sekta za maendeleo zikiwemo elimu, kilimo, miundo mbinu ya usafiri pamoja na kuondoa malumbano ili kuwaunganisha wazanzibari kuwa kitu kimoja.

Wamesema Zanzibar bado inakabiliwa na changamoto za kiuchumi hivyo watajenga mazingira mazuri ikiwani pamoja na kuimarisha sekta za kazi ili kutoa huduma nzuri pamoja na kubuni nafasi za ajira.

Aidha viongozi hao wamesema wataendelea kuimarisha muungano ili kuleta mafanikio zaidi kwa wananchi na kuendelea kuyapatia fumbuzi baadhi ya matatizo yaliosalia kwa lengo la kuleta maslahi kwa pande zote mbili.

Akizungumza mara baada ya kuwakabidhi fomu wagombea hao katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, Vuai Ali Vuai amesema kamati kuu ya halamshauri itapitia sifa za wagombea hao na kutoa mapendekezo yake kwa majina matatu kwa halmashauri kuu ya taifa kwa uteuzi wa mwisho…

Afisi kuu ya CCM bado inaendelea kutoa fomu kwa wanachama wengine wanaotaka kuwania urais wa Zanzibar kupitia chama hicho hadi Julai mosi mwaka huu.

Idadi hiyo ya wananchama waliojitokeza kuchukua fomu ya kukiomba chama chao kuwateuwa kugombea nafasi ya urais wa Zanzibar ni kubwa ikilinganishwa na wanachama waliojitokeza kumrithi rais wa zamani Dr. Salmin Amour Juma mwaka 2000.

Wachambuzi wa masuala ya siasa Zanzibar wanasema uchaguzi wa rais mwaka 2010 utakuwa na upinzani mkali na vyama vikuu viliwi vya siasa vyenye wafuasi wengi CCM na CUF vitahitaji kufanya kazi ya ziada.

No comments:

Post a Comment