UWAIT imeahidi kuendelea kuinga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu kutokana na mafanikio makubwa yaliopatika sanjari na mikakati madhubuti iliyojiwekea katika kuimarisha sekta hiyo.
Mjumbe wa Bodi wa Afrika Muslim Agency kutoka Kuwait ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Juu la Chuo Kikuu cha Elimu Zanzibar Dk. Abdulrahman Saleh Muhailan akiwa na ujumbe wake aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume.
Katika maelezo yake Dk. Saleh alimueleza Rais Karume kuwa Kuwait inathamini sana juhudi za Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta ya elimu na kuahidi kuongeza nafasi za masomo kwa Wazanzibar nchini humo.
Alieleza kuwa hatua hiyo inatokana na Kuwait kuwa na uhusiano na ushirikiano wa muda mrefu kati yake na Zanzibar.
Alisema kuwa tayari Afrika Muslim Agency imekuwa ikiendelesha shughuli za elimu kwa muda mrefu na kuweza kuwa na vyuo vingi na skuli katika nchi mbali mbali za bara la Afrika ikiwemo Zanzibar.
Dk. Saleh alimueleza Rais Karume kuwa Chuo Kikuu cha Elimu Zanzibar kinathamini sana ushirikiano uliopo kati yake na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar hali ambayo imepelekea kuendelea kupata mafanikio zaidi katika chuo hicho.
Pamoja na Dk. Saleh alimkabidhi Rais Karume hati yenye ‘password’ kwa ajili ya kutumia vitabu vilivyopo katika Maktaba ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Gulf kiliopo nchini Kuwait.
Dk. Saleh alimueleza Rais Karume kuwa hatua hiyo itawasaidia wanafunzi wa Zanzibar kupata kusoma vitabu, majarida na taarifa mbali mbali kutoka Maktaba hiyo kwa njia ya Mtandao.
Nae Rais Karume kwa upande wake alitoa shukurani kwa kiongozi huyo pamoja na nchi ya Kuwait kwa kuendeleza ushirikiano na uhusiano wa kihistoria uliopo kati ya nchi mbili hizo.
Rais Karume alisema kuwa Zanzibar ina historia refu na Kuwait hatua ambayo imeweza kuimarika hadi leo hii.
Alisema kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imo katika kuimarisha sekta ya elimu ambayo tayari imeshapata mafanikio makubwa.
Rais Karume alisema kuwa mbali ya sekta ya elimu, tayari sekta mbali mbali za maendeleo hapa nchini zimeweza kupata mafanikio na kupiga hatua kubwa kimaendeleo.
Aidha, Rais Karume alieleza kuwa kutokana na juhudi zinazochukuliwa na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo ikiwemo sekta ya elimu imekuwa chachu kwa washirika wa maendeleo kuendelea kuiunga mkono Zanzibar.
Rais Karume alieleza kuwa hivi Karibuni Serikali ya Mapinduzi Zanzibar imetiliana saini na Shirika la Misaada la Marekani (USAID) kwa ajili ya kuziunganisha skuli zote za Unguja na Pemba katika mtandao hivyo hatua ya Taasisi ya Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia cha Gulf nchini Kuwait ya kusaidia njia ya kupata kusoma vitabu kutoka maktaba yao kutawasaidia kwa kiasi kikubwa wanafunzi wa Zanzibar.
Sambamba na hayo Rais Karume aliipongeza Afrika Muslim Agency kwa kuendeleza sekta ya elimu na kuweza kuzisaidia kwa nguvu zake zote nchi mbali mbali za Bara la Afrika katika kuimarisha sekta ya elimu.
Pamoja na hayo, Rais Karume aliueleza uongozi huo kuwa Zanzibar inathamini sana mashirikiano hayo yaliopo katika sekta ya elimu na sekta nyengine ambapo imekuwa ikiziunga mkono hapa nchini
Wednesday, June 16, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment