RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume amesema kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar zote kwa pamoja zimepanga mikakati maalum kwa ajili ya kuwapunguzia wananchi wake makali ya umasikini.
Rais Karume aliyasema hayo leo katika ufunguzi wa Mkutano wa Kimataifa kuhusu miradi ya jamii kwa nchi zinazoendelea unaofanyika katika ukumbi wa Mkutano wa AICC Mjini Arusha.
Rais Karume ambaye alimuwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungani wa Tanzania Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete, alieleza kuwa Serikali zote mbili za Tanzania zinatambua umuhimu wa kuanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), ambao huwashirikisha wadau wengi.
Alieleza kuwa katika kipindi chote ambacho TASAF imekuwa ikifanya kazi jumla ya miradi 11,375 ya jamii imepatiwa misaada kutoka mfuko huo wenye thamani ya Dola za Kimarekani 164,446,823.
Rais Karume alieleza kuwa kati ya miradi yote iliyopata misaada kutoka TASAF 928 ilikuwa ni kwa ajili ya kazi za kijamii yenye thamani ya Dola za Kimarekani 21,422,495.28 iliyowanufaisha jumla ya watu 217,315.
“Tokea kuanzishwa kwa TASAF tayari umeshawanufaisha watu 15,320,58 ambao wameweza kuzitumia huduma zilizotolewa baada ya kukamilika kwa miradi ya kijamii katika maeneo yao”,alieleza Rais Karume.
Aidha, Rais Karume alisema kuwa TASAF imekuwa ikifanya kazi vizuri Zanzibar na tayari imeshatoa kiasi cha Dola za Kimarekani 2.50 milioni kwa ajili ya kusaidia miradi mbali mbali maendeleo katika awamu ya pili iliyoanza mwaka 2005.
Pia, Rais Karume iliisifu TASAF kwa misaada midogo midogo inayotolewa kutoka katika Mfuko huo.
“Mahitaji ya familia yanaongezeka lakini kipato hakiongezeki, kutokana na sababu hii Serikali ya Tanzania imetambua umuhimu wa kuanzisha mfuko wa Mandeleo ya Jamii (TASAF), ambapo matatizo mbali mbali yanayozikabili jamii yamekuwa yakishughulikiwa kwa kiasi kikubwa”,alisisitiza Rais Karume.
Alieleza kuwa Mpango wa Maendeleo wa muda mrefu wa Dira ya 2025 kwa Tanzania Bara na ule wa 2020 kwa Zanzibar unatambua umuhimu wa kuwawezesha watu mbali mbali katika makundi tofauti wakiwemo wale wanaoishi katika mazingira magumu.
Akihutubia katika mkutano huo unaohudhuriwa na wajumbe kutoka nchi 45 duniani, Rais Karume alisema kuwa mkutano huo unafanyika wakati dunia ikiwa katika jitihada kubwa ya kutatua matatizo yaliyojitokeza kutokana na kutetereka kwa uchumi na mfumo wa fedha wa duniaambao umeathiri shughuli za kibiasahara na kushuka kwa sekta ya uwekezaji duniani.
Rais Karume alieleza kuwa pale uchumi wa dunia unaposhuka matatizo yanayotokea katika mataifa makubwa yenye nguvu za kiuchumi athari zinazotokezea huzikumba na nchi ndogo..
Alieleza kuwa miongoni mwa athari hizo ni pamoja na kuwepo kiwango kidogo cha uwekezaji na kutetereka kwa sekta ya Utalii ambapo nako kumechangia kushuka kwa soko la ajira na mapato ya serikali ambapo pia, imepelekea kuathiri utekelezaji wa ujenzi wa miundombinu ya kijamii.
Nae Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Utawala Bora Mhe. Sophia Simba alieleza kuwa TASAF imekuwa na umuhimu mkubwa katika kuimarisha shughuli za maendeleo ya kijamii hapa Tanzania na kuishukuru Benki ya Dunia kwa uwamuzi wake wa kufanya mkutano wake huo muhimu hapa nchini.
Mkurugenzi Mkaazi wa Benki ya Dunia kwa nchi za Tanzania, Uganda na Burundi Bwana John Murray McIntire alieleza kuwa Benki ya Dunia itaendelea kuunga mkono katika kufanikisha Miradi ya TASAF kwa kutambua umhimu wake katika maendeleo ya jamii.
Alieleza kuwa miongoni mwa nchi zilizopata mafanikio katika Mfuko huo wa TASAF ni pamoja na Tanzania ambayo imeweza kuimarisha miradi mbali mbali ya maendeleo.
Wakati huo huo Rais Karume alikagua maonyesho yaliyotayarishwa na TASAF na kuona jinsi mfuko huo unavyofanya kazi kutokana na maelezo aliyokuwa akipewa na watayarishaji husika
Wednesday, June 16, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment