I made this widget at MyFlashFetish.com.

Thursday, August 5, 2010

UN YATOA PONGEZI KWA ZANZIBAR

UMOJA wa Mataifa umetoa pongezi zake kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Amani Abeid Karume na wananchi wote wa Zanzibar kwa kufanikisha kura ya maoni kwa amani na utulivu.

Naibu Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Dk. Asha-Rose Migiro aliyasema hayo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais Karume, Ikulu mjini Zanzibar.

Dk. Migiro, alimueleza Rais Karume kuwa Umoja wa Mtaifa umeridhika na hatua iliyofikiwa katika kufanikisha zoezi zima la kura ya maoni kwa amani, utulivu na mafanikio makubwa.

Akitoa salamu za Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Ban Ki-moon, Dk. Migiro alieleza kuwa, UN imeridhishwa na makubaliano yaliyofanyika kati ya Rais Karume kupitia chama cha CCM na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad kwa lengo la kuondosha kabisa migogoro iliyokuwepo hapo kabla.

Katika salamu hizo, Ban Ki-moon aliwatakia kila la heri wananchi wa Zanzibar katika kujenga amani na umoja ambao utawasaidia katika kufikia lengo lililokusudiwa ambapo UN itaendelea kutoa ushirikiano wake ili kuweza kupata mafanikio zaidi.

Katibu Mkuu huyo wa UN, aliipongeza Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kwa kuweza kusimamia vyema zoezi hilo kwa salama na amani.

Aidha, Dk. Migiro alimueleza Rais Karume kuwa UN imefarajika kwa namna Serikali anayoiongoza Rais Karume inavyotoa mashirikiano yake kwa Umoja huo sanjari na Mashirika yake yaliopo hapa Zanzibar.

Dk. Migiro alimueleza Rais Karume kuwa licha ya kumaliza muda wake wa Urais yeye mwenyewe binafsi pamoja na UN hautamsahau Rais Karume kwa juhudi zake kubwa alizozifanya katika uongozi wake ikiwa ni pamoja na kuwaletea wananchi wa Zanzibar maendeleo makubwa.

Sambamba na hayo, Dk. Migiro aliipongeza Zanzibar kwa kuendelea kuunga mkono Umoja wa Mataifa.

Nae Rais Karume alitoa shukurani zake kwa UN na kueleza kuwa mashirikiano mazuri yamekuwa yakipatika kutoka Umoja huo kupitia mashirika yake yaliopo nchini yakiongozwa na UNDP.

Rais Karume alieleza kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inajivunia mashirikiano na uhusiano mwema unaoupata kutoka Umoja wa Mataifa ambapo alieleza kuwa hata katika mafanikio yaliopatikana kwenye zoezi la kura ya maoni Shirika la Maendeleo la UNDP lilitoa ushirikiano wake mkubwa katika ufanikishaji.

Katika maelezo yake, Rais Karume alisema kuwa Umoja wa Mataifa umekuwa karibu sana na Zanzibar katika kutoa mashirikiano yake kwenye kuimarisha miradi ya maendeleo na uchumi.

Akieleza juu ya mafanikio yaliopatikana katika kura ya maoni, Rais Karume alisema kuwa mafanikio ya kura ya maoni kwa Wazanzibari wote kwani lengo na madhumuni ni kuimarisha umoja,mshikamano sanjari na amani na utulivu.

Sambamba na hayo, Rais Karume alimueleza Naibu Katibu Mkuu huyo wa UN kuwa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, inayokusudiwa kuundwa baada ya Uchaguzi Mkuu ujao ni ya wananchi wote wa Zanzibar.

Rais Karume alieleza kuwa Zanzibar imepata mafanikio kiuchumi, kisiasa na kijamii kutokana na mashirikiano mazuri yaliopo nchini, hivyo mafanikio hayo yataimarishwa zaidi kwa kukuza na kuimarisha umoja na mshikamano miongoni mwa Wazanzibari.

Rais Karume alisema kuwa wananchi wa Zanzibar wamepiga hatua kidemokrasia hali ambayo imeonekana kutokana na maamuzi na mapendekezo yao waliyoyatoa katika kuimarisha umoja na mshikamano.

Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alimueleza Naibu Katibu Mkuu huyo kuwa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na wananchi wake wanaipongeza UN chini na uongozi wa Bwana Ban Ki-moon kwa mashirikiano mazuri na uhusiano mwema unaotoa kwa Zanzibar.

No comments:

Post a Comment