UMOJA wa nchi za Ulaya (EU) umetoa pongezi kwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dk. Amani Abeid Karume kutokana na kufanikisha zoezi la Kura ya Maoni na kueleza kuwa Zanzibar imepata maendeleo ya kupigiwa mfano kidemokrasia.
Mwakilishi wa Umoja wa nchi za Ulaya, Balozi Tim Clarke aliyasema hayo leo wakati alipokuwa na mazungumzo na Rais Karume Ikulu mjini Zanzibar.
Katika mazungumzo hayo ambapo Balozi Clarke akifuatana na baadhi ya Mabalozi wa nchi za Ulaya wanaofanyia kazi zao hapa Tanzania, alisema kuwa hatua iliyofikiwa Zanzib ar katika demokrasia ni kubwa na inapaswa kuungwa mkono.
Alisema kuwa Umoja wa nchi za Ulaya umeridhishwa na hatua hiyo na kutoa pongezi zake kwa Rais Karume pamoja na Wazanzibari wote kwa jumla kutokana na mafanikio makubwa waliyoyapata katika kuimarisha demokrasia.
Bwana Clarke na ujumbe wake walimueleza Rais Karume kuwa wanamatarajio makubwa kuwa Zanzibar itazidi kupiga hatua katika kuimarisha maendeleo yake sanjari na kudumisha umoja na mshikamano miongoni mwa wananchi wake hali ambayo itaipaisha Zanzibar katika medani na kiuchumi, kisiasa na kijamii.
Mwakilishi huyo, alimueleza Rais Karume kuwa ulimwengu mzima kwa namna zoezi hilo lilivyoendeshwa na hatimae kumalizika kwa ufanisi.
Katika mazungumzo hayo, viongozi hao walimueleza Rais Karume kuwa wameridhika na kuvutika kwa namna ya zoezi zima la Kura ya Maoni lilivyokwenda vizuri na kuwa ulimwengu mzima umefurahishwa na namna lilivyokwenda kwa amani na utulivu.
Walieleza kuwa EU itaendelea kutoa mashirikiano yake na Zanzibar kwa na kueleza kuwa wanamatumaini makubwa kuwa Umoja na mshikamano wa Wazanzibari utaendelea kuimarika zaidi.
Aidha, viongozi hao, walimueleza Rais Karume kuwa ni kiongozi anaependa umoja, mshikamano sanjari na kuimarishaji amani na utulivu hapa nchini kwa lengo la kuiletea Zanzibar maendeleo na maisha yenye utulivu.
Sambamba na hayo, viongozi hao waliwatakia Wazanzibari wote pamoja na viongozi wao wa kisiasa kuendelea kupata mafanikio katika kutekeleza umoja huo kwa lengo la kuleta maendeleo endelevu kwa wananchi na nchi yao kwa jumla.
Viongozi hao waliahidi kushirikiana bega kwa bega na Zanzibar katika kuhakikisha mafanikio zaidi yanapatikana katika kuimarisha sekta za maendeleo kutokana na kuthamini juhudi inazozichukua katika kufikia hatua hiyo..
Nae, Rais Karume kwa upande wake aliwaeleza viongozi hao wa EU kuwa zoezi la kura ya maoni ni la kihistoria ambalo limewapa wananchi wa Zanzibar haki ya kushiriki kikamilifu katika maamuzi wanayohisi yatawaletea manufaa zaidi.
Alieleza kuwa katika zoezi hilo la Kura ya Maoni hakuna alieshinda na aliyeshindwa kwani washindi ni Wazanzibari wote ambao wanapenda amani, umoja na mshikamano.
Rais Karume alieleza kuwa mafanikio ya zoezi hilo yamedhihirisha wazia kuwa Wazanzibari wamepevuka kisiasa.
Rais Karume alisema kuwa Wazanzibari wote wanapenda umoja, mshikamano sanjari na amani na utulivu na ndio maana wameunga mkono ili kutimiza na kuendeleza malengo yao hayo.
“Watu wote wa Zanzibar wanapenda amani”,alisema Rais Karume. Aidha, Rais Karume alisema kuwa kwenda vizuri kwa zoezi hilo kunatokana na taratibu nzuri zilizowekwa na Tume husika sanjari na wananchi wenyewe kuwa na mwamko na uwelewa juu ya zoezi hilo.
Katika mazungumzo hayo, Rais Karume alisema kuwa kufanikiwa kwa zoezi hilo kutatoa matokeo mazuri ambayo yataijenga Zanzibar mpya na yenye amani, umoja na mshikamano.
Rais Karume alitoa pongezi na shukurani kwa Washirika wa Maendeleo zikiwemo nchi za Umoja wa Ulaya kwa kuendelea kuiunga mkono Zanzibar katika kuimarisha sekta zake za maendeleo sanjari na kuunga mkono zoezi la Kura ya Maoni lililofanyika Julai 31 mwaka huu.
Thursday, August 5, 2010
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment