I made this widget at MyFlashFetish.com.

Monday, November 1, 2010

MGOMBEA WA URAIS WA ZANZIBAR ANAONGOZA KATIKA MAJIMBO 12 YA MJINI MAGHARIBI

Chama cha mapinduzi CCM kinaongoza katika kura za urais wa Zanzibar kwenye majimbo 12 kati ya 15 ya mkoa wa mjini magharibi, huku chama cha wananchi CUF kikiongoza katika majimbo matano ya wilaya ya Wete.

Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Zanzibar Khatib Mwinyichande amesema mgombea wa CCM Dr. Ali Mohammed Shein ameshinda katika majimbo ya Fuoni, Dole, Dimani, Kiembesamaki, Mwanakwerekwe, Bububu, Mfenesini na Mpendae.

Majimbo mengine aliyoshinda Dr. Shein ni Amani, Rahaleo, Kikwajuni na Kwahani wakati mgombea wa CUF Seif Sharif Hamad ameshinda katika majimbo ya Mtoni, Magogoni na Mji Mkongwe.

Wagombea wengine wa vyama vya AFP, TADEA, NCCR-MAGEUZI, NRA, JAHAZI ASILIA na TADEA wamepata kura chini ya asilimia mbili katika majimbo hayo.

Na huko kisiwani Pemba mwandishi wetu alioko katika afisi ya uchaguzi wilaya ya Wete amesema kwa mujibu wa matokeo yaliotolewa na afisi hiyo kwa majimbo ya Kojani, Wete, Konde, Gando na Mtambwe, mgombea wa CUF Hamad anaongoza katika majimbo hayo…

Tume ya uchaguzi Zanzibar imesitisha kwa muda kutangaza matokeo ya urais wa Zanzibar katika majimbo yaliobakia hadi saa 3.00 asubuhi hii, lakini matokeo ya uwakilishi na udiwani yameanza kutangazwa katika afisi za uchaguzi za wilaya.

Uchaguzi mkuu wa Zanzibar wa mfumo wa vyama vingi kwa mara ya kwanza umefanyika kwa amani na utulivu ikilinganishwa na chaguzi tatu zilizopita.

No comments:

Post a Comment